Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Mbaraka Alhaji Batenga amewaonya wananchi wote wa wilaya ya Chunya kuhusisha Daftari la Mkaazi la Kitongoji na Mambo ya Kisiasa jambo linalosababisha watu wengi kutojiandikisha kwenye Daftari la Kitongoji, hivyo awamewataka wanachunya kuhakikisha wamejiandikisha kwenye Madaftari ya Kitongoji ili kurahisisha wananchi kutambuana wao kwa wao lakini kurahisisha ufuatiliaji linapotokea tatizo lolote kwenye jamii.
Ametoa onyo hilo tarehe 04/12/2024 wakati akitoa salamu za Serikali kwenye ibada ya kuaga mwili wa Ndugu Michael Kalinga aliyeuawa usiku wa kuamkia tarehe 3/12/2024 katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa la Moraviani Usharika wa Makongolosi, Chunya
“Sasa niwaombe ndugu zangu Chunya mnaifahamu, Chunya ni salama, wanachunya ni watu waungwana. Hawa watu wanatoka wanakotoka na bahati mbaya tunaishi nao hata hatuhoji, Ndugu zangu tuendelee kutambuana maeneo tunayoishi, Tuna Daftari la Mkazi kwenye maeneo yetu, watu wanachukulia daftari hilo ni jambo la kisiasa, Tuacheni mambo hayo. Daftari hilo linalenga kumtambua nani ni nani na anaishi wapi, anafanya gani?. Kamuulize Jirani yako umejiandikisha kwenye Daftari la kitongoji unachoishi? Kama hajajiandikisha muhimize akajiandikishe ili tuweze kujuana na kupata eneo la kuanzia linapotokea tatizo na msione ni kazi nyepesi kuanza kutafuta muuaji aliyemuua Michael saa tano usiku Chunya kata ya Bwawani na akakamatwe Mbozi sio kazi ndogo, lakini tungekuwa tutambuana ingekuwa kazi nyepesi sana” Alisema Mhe Batenga
Aidha Mhe Batenga amewapongeza Jeshi la polisi na Vyombo vyote vya usalama kwa Juhudi kubwa waliyoifanya kuhakikisha watuhumiwa wa Mauaji ya Michael Kalinga wanakamatwa, Huku akiwataka kuendelea na juhudi na moyo wa kazi hivyo hivyo ili waendelee kuwahudumia wananchi wa Chunya na Watanzania kwa ujumla na kupitia Juhudi hizo wananchi wataendelea kuiamini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
“Sisi tulipopata taarifa hizi tuliingia kazini wakati huo huo, sasa niwape taarifa ndugu zangu, Tulianza kazi tangu juzi saa tano usiku tulipoata taarifa mpaka nasimama mbele yenu tumewakamata watuhumiwa wawili pamoja na pikipiki waliyoiiba ya Ndugu yetu Michael Kalinga. Ndio Maana tunasema tuendelee kuiamini serikali ya awamu ya sita Chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan, unaweza usielewe kama mambo hayajaharibika lakini mambo yakiharibika ndipo utajua Serikali inafanya kazi” Aliongeza Mhe Batenga
Mwenyekiti wa Jumuhiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Ndugu Mohamed Ally Kawaida alisema vijana wa Chama cha Mapinduzi wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Kijana mwenzao huku akisema sifa njema za Marehemu zimemfanya asafiri kuja kuungana na familia, wanachunya na Watanzania wote kumsindikiza kwenye Nyumba yake ya Milele.
“Sifa Njema za Kijana huyu, Mashirikiano yake mazuri ambaye kwa sasa ni Marehemu nimezipata kupitia Mwenyekiti wangu wa Vijana Mkoa, nami nikasema nifunge safari kutoka Dar es Salaam mpaka Mbeya kwa Gari maana muda niliopata taarifa ulikwa umeshaenda hivyo nikasema nije niungane nanyi ndugu zangu wa Chunya. Mimi ni baba na ni Mume hivyo natambua mateso, maumivu wanayopitia Familia yake kwa maana ya Mke, watoto, Wazazi na hata wale wafuasi wake pia nambua huzuni na upweke ambao jamii iliyokuwa inamzunguka inakutana nao, hivyo niwape pole. Jeshi la polisi la wilaya ya Chunya likiongozwa na wewe mkuu wa wilaya hizi ni habari njema lakini nisisitize kwa Jeshi la polisi na vyobo vingine vya usalama vichukue hatua kwa mambo haya yanayoendelea kwenye nchi ya utekaji na uuaji na pindi mnapopata taarifa basi rudisheni kwa wananchi ili wajue nini kinaendelea”. Alisema Ndugu Kawaida
Msiba wa Ndugu Michael Kalinga aliyezaliwa mwaka 1986 na umauti kumfika mwaka 2024 umehudhuriwa na viongozi Mbalimbali wakiwepo viongozi wa Dini wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya, Serikali, huku vijana wa Chama Cha Mapinduzi wakiongozwa na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Ndugu Mohamed Kawaida wakiungana na wananchi wengine kumsindikiza Kijana huyo kwenye Nyumba yake ya Milele
Mwenyekiti wa Jumuiya ya umoja wa vijana Taifa Ndugu Mohamed Kawaida akiwasilisha salamu za Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa wakati wa Ibada ya Kuaga mwili wa Kijana mwenzao Ndugu Michael Kalinga ndani ya kanisa la Moraviani Usharika wa Makongolosi Chunya
Mbunge wa Jimbo la Lupa Mhe Masache Njelu Kasaka akitoa salamu wakati wa Ibada ya kuaga mwili wa Michael Kalinga tayari kuelekea kwenye mapumziko ya Milele
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na katibu wake wakiweka Shada ishara ya kumuaga Mwanachama na kiongozi katika Chama chake wakati wa kumsindikiza kwenye Nyumba yake ya Milele
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.