Halmashauri ya wilaya ya Chunya imechomoza kinara katika Mkoa wa Mbeya katika zoezi la chanjo ya Polio kwa watoto chini ya Miaka mitano ambalo limefanyika nchi nzima ambapo imechanja watoto 91,501 sawa na asilimia 160 huku wilaya inayofuatia ikiwa na asilimia 132 ya lengo lililokusudiwa huku lengo la chanjo hiyo likiwa ni kuepukana na athari zinazoweza kujitokeza kwa wananchi endapo ugonjwa huo utakapowakumba wananchi ambao umeonekana maeneo ya karibu na Nchi yetu.
Mratibu wa Chanjo Halmashauri ya wilaya ya Chunya ndugu Blasio N. Kabwebwe amesema zoezi hilo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na kwanza maandalizi sahihi yaliyofanyika kabla ya zoezi kuanza, ushirikiano wa viongozi wote katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya, bidii na kujituma kwa wataalamu walioshiriki katika zoezi hilo na hata utayari wa wananchi baada ya kupewa Elimu juu ya Umuhimu wa chanjo hiyo.
“Wilaya yetu imekuwa kinara katika zoezi la Chanjo ya Polio awamu hii kwasababu kwanza maandalizi tuliyoyafanya kabla ya Chanjo hiyo kwa maana ya elimu kwa wataalamu, wananchi na viongozi wa serikali, pili ushirikiano ambao tunaupata kutoka kwa viongozi wote wa wilaya ya Chunya kwa ngazi zote lakini pia bidii na kujituma kwa wataalamu wote walioshiriki zoezi zima na mwisho ingawa sio kwa umuhimu ni utayari wa wananchi wetu kushiriki zoezi hilo maana bila utayari wao tusingefanikiwa kwa kiwangon hicho”
Mganga Mkuu wa wilaya ya Chunya Dr Darson Andrew amesema Chunya inafanya vizuri sio kwenye chanjo ya Polio awamu hii tu bali pia chanjo zote na utekelezaji wa afua mbalimbali ikiwepo afua za lishe ambapo kwa awamu hii Chunya ilishika nafasi ya tatu kitaifa na kwa maana hiyo Halmashauri yetu iliongoza mkoa na ameongeza kuwa kwa namna ambavyo viongozi wanavyowapatia ushirikiano basi Chunya itaendelea kufanya vizuri
“Sisi Chunya tunafanya vizuri maeneo mbalimbali sio Chanjo ya Polio tu, hivi karibuni Chunya imepata nafasi ya tatu kitaifa kwa utekelezaji wa mkataba wa lishe nchini na kwa maana hiyo Chunya iliongoza Mkoa katika eneo hilo na kwa namna tunavyopata ushirkiano toka ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Chunya, Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji, Madiwani kupitia kwa Mwenyeki wa Halmashauri na viongozi wengine wote Chunya tutaendelea kufanya vizuri zaidi”
Wataalamu walioshiriki kuhakikisha zoezi linafanikiwa wamesifu namna ambavyo waratibu na viongozi kwa ujumla walivyowapatia ushirikiano katika kutatua changamoto kabla ya zoezi, wakati wa zoezi na hata katika hatua za mwisho za kukamilisho kazi hizo jambo ambalo wametaja kuwaongezea morali ya kufanya kazi kwa bidii na weledi na hatimaye kuvuka lengo lililokusudiwa
Zoezi la Chanjo ya polia kitaifa limefanyika kuanzia tarehe 21-24/9/2023 ambapo halmashauri ya wilaya ya Chunya ililenga kuchanja watoto 56,979 lakini imefanikiwa kuchanja watoto 91,501 ambao ni sawa na asilimia 160 hivo Chunya kuvuka lengo kwa zaidi ya asilimia 60 ya lengo lililokusudiwa kufikiwa.
Afisa wa Afya katika kata ya Mafyeko akitoa Chanjo eneo la Mnada wakati wa Chanjo ya Polio iliyofanyika Nchi nzima kuanzia tarehe 21-24 september 2023
Namna wananchi katika kata ya Ifumbo walivyoitikia wito wa chanjo ya Polio baada ya kuelimisha juu ya umuhimu wa Chanjo hiyo
Baadhi ya wahudumu waliohusika katika zoezi la Chanjo ya Polio wakiwa kwenye Mafunzo ya namna ya kutekeleza jukumu hilo anayetoa maelekezo ni Mganga Mkuu wa wilaya ya Chunya Dr Darson Andrew wakati wa mafunzo kujiandaa na zoezi la Chanjo ya Polio
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.