Mara zote kazi na jukumu la Serikali yoyote makini na inayowajali wananchi wake popote pale duniani ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa wananchi wake ili kufanya shughuli mbalimbali za kuwapatia kipato kwa urahisi na wepesi
Mazingiara yanayotengenezwa na Serikali hayabagua kiwango cha Elimu alichonacho mtu mmoja mmoja, bali wananchi wote bila kujali utofauti wa elimu, vipato kwa Pamoja ruksa kushiriki katika shughuli za kujiingizia kipato
Serikali ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya imekuwa ikitekeleza na kuishi falsafa ya kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi wake ili waweze kujishughulisha katika shughuli mbalimbali za kujipatia kipato.
Ni raasmi sasa Chunya zao la ufuta kuwa moja kati ya vyanzo vya kuwapatia kipato watanzania waishio Chunya na Tanzania kwa ujumla kwani fursa sasa zimefunguka
Makala hii imeandaliwa na Joshua Sengo kutoka Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Halimashauri ya wilaya ya Chunya
Baada ya Mafanikio makubwa ya usimamizi wa zao la Tumbaku Chunya na kuleta tija kubwa kwa wakulima na Halmashauri, sasa ni rasmi kilimo cha ufuta Chunya Fursa Mpya yenye lengo la kuendelea kuchagiza mabadiliko na maendeleo ya wananchi wa Chunya na hatimaye Taifa kwa ujumla
Kwa dhati kabisa Serikali wilayani Chunya imekuwa ikitanguliza maslahi ya wananchi wake katika mipango yake huku utekelezaji ukiwa shirikishi kwa kila ngazi na kila hatua
Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Bibi Janeth Mwaigoga anaeleza vipaumbele vya Halmashauri kwa Baraza la Madiwani wakiwawakilisha wananchi wao lengo likiwa ni kuendeleza uwazi katika utekelezaji wa Serikali

Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Bi Janeth Mwaigoga akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti wakati wa Baraza Maalumu la Bajeti
“…namba moja ni kutenga fedha kwaajili ya kuviwezesha vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu kwa maana ya asilimia 10, namba mbili ni kuboresha huduma za kijamii kwa maana ya afya na Elimu, Kipaumbele cha tatu ni Kuongeza ukusanyaji wa Mapato kwa kutumia mifumo ya Machine za kielektroniki, kipaumbele cha nne kuboresha miundombinu ya maendeleo na kuongeza uwekezaji wa viwanda kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi, lakini kipaumbele cha tano ni kutoa huduma za ugani kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji kwa mazao ya kilimo na migugo” Alisema Bi Mwaigoga
Mkuu wa Divisheni ya Mipango na uratibu amesema Serikali wilayani Chunya imeendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ya Halmashauri lakini pia kuongeza usimamizi kwenye shughuli za ugani hivyo tayari zao la Ufuta limeguswa moja kwa moja katika vipaumbele
Wakati vipaumbele vikitajwa na Mkuu wa Divisheni ya Mipango na uratibu, Mkurugenzi mtendaji kwa upande mwingine anaendelea kuzungumza na wadau ili kuungana nao katika usimamizi wa soko la ufuta ili wananchi waweze kunufaika

Wadau wa zao la Tumbaku wilaya ya Chunya wakiwa kwenye Mkutano Mkuu wa 26 wa mwaka 2026 uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Omary City Hotel
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya ndugu Tamim Kambona kupitia kikao cha Chama Kikuu cha ushirika 2026 aliwaomba Chama Kikuu cha Ushirika Chunya (CHUTCU) kusimamia mchakato wa ununuaji na uuzaji wa ufuta mwaka huu 2026
Mkurugenzi mtendaji amejilidhisha na usimamizi mzuri wa Chama Kikuu cha ushirika katika mchakato mzima wa zao la Tumbaku hivyo amewaomba CHUTCU kusimamia soko la ufuta huku akiwa na uhakika kwamba wakulima watanufaika kwa usimamizi huo

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Ndugu Tamim Kambona wakati akizungumza na wadau wa Tumbaku wakati wa Mkutano wa 26 wa Mwaka 2026
“Lakini kama mlivyokuwa mnajadiliana na sisi kule tumejadiliana suala la ufuta kusimamiwa na CHUTCU, Mimi niombe mkazo uwekwe haraka ili zao hili la ufuta lisimamiwe na CHUTCU, Nimesikia changamoto za Maghala na mimi pale najenga ghala niko tayari kuwakabidhi ghala lile ili mtumie kwaajili ya kununulia ufuta kwani usimamizi wenu unatunufaisha sote” Alisema Kambona
Pamoja na Juhudi kubwa za Viongozi Chunya, Wakulima wengi kutoka maeneo mbalimbali ya Chunya wakiwakilishwa na Christiani Ntaly, Emanuel Mwakitega, Hassan Mlaga na wengine wamesema bado elimu kuhusu kilimo cha Ufuta haijawafikia ipasavyo huku wengine wakiamini maeneo yao sio rafiki sana kwa kilimo Cha zao la ufuta
Aidha wakulima wa Chunya hawajawahi kuacha fursa ipite, hivyo wamesema wako tayari kulipokea zao la ufuta na kutumia fursa hiyo kujipatia kipato ikiwa watapatiwa Elimu ya kutosha
Kuanzishwa kwa Chama cha Msingi cha wakulima wa Ufuta Chunya ni ishara tosha kwamba sasa ufuta Chunya ni fursa Mpya kwa wananchi wa Chunya huku Changamoto za Elimu zikipatiwa suluhu kwa pamoja
Mwenyekiti wa Chama Cha Msingi cha wakulima wa Ufuta Chunya ndugu Peter Mayala anaeleza hali ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa chama Cha ushirika cha wakulima wa Ufuta Chunya huku akikiri wazi mabadiriko yenye tija kwa wakulima wa Chunya

Mwenyekiti wa Chama Cha Msingi cha wakulima wa zao la Ufuta KILIMO KWANZA AMCOS Ndugu Peter Mayala akifafanua jambo
Aidha Bwana Peter Mayala kwa niaba ya wakulima wa Ufuta Chunya amewashukuru kwa dhati viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya kwa ujumla wake kwa namna wanavyoshirikiana nao katika kila hatua
Mwenyekiti huyo anawahimiza wakulima kuzingatia maelekezo ya viongozi wao huku akiendelea kushukuri ujenzi wa miundombinu wezeshi ya soko kwa kujenga maghala yanayoendelea kurahisisha soko la ufuta.
Makala hii imemtafuta Mkuu wa divisheni ya Kilimo, mifugo na uvuvi Halmashauri ya wilaya ya Chunya ndugu Gidion Mapunda kutaka kufahamu uzalishaji wa zao la ufuta kwenye wilaya ya Chunya ukoje.
Makala hii pia imetaka kujua namna ambavyo wakulima wamenufaika kupitia zao la ufuta katika msimu wa 2024/2025 kwani ndio kwa mara ya kwanza soko la ufuta rasmi kufanyika Chunya

Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Ndugu Gidion Mapunda akifafanua jambo akiwa ofisini kwake
Bwana Mapunda ameeleza mpango wa Halmashauri kwenye kilimo cha Ufuta, huku akiwahakikishia wananchi wa Chunya kundelee kujitokeza kushiriki kwenye mnyororo wa uzalishaji wa ufuta ili kujiongezea kipato kwani Serikali itaendelea kuhakikisha mazingira ya uzalishaji wa ufuta yanaendelea kuboreshwa
“…kwa mwaka wa fedha 2024/2025 zao la ufuta limefanya vizuri sana, tulipofungua soko tukakusanya kiliomo miliomi mbili laki mbili na sabini na saba elfu na mia tatu hamsini (2,277,350) ambazo zilipelekea na mzunguko wa Zaidi ya bilioni tano (5,179,367,750/=). Na kwa uelewa tu ni kwamba kata zote za wilaya ya Chunya zinaweza kulima ufuta kwani ufuta hulima kwenye eneo lenye mvua ya wastani na joto la wastani” Alifafanua Ndugu Mapunda
Mapunda ametoa rai kwa wakulima kujali shughuli zao za kilimo kama wanavyojali shughuli nyingine huku akiwataka kuwatumia wataalam wa ugani waliopo kwenye maeneo yao, huku Mapunda amewaagiza wataalam wa ugani wote Chunya kuweka mawasiliano yao kwenye mbao za Matangazo ili wakulima wanapokuwa na shida wawatafute na kuwapata kwa haraka ili kuleta suluhu katika mchakato mzima wa uzalishaji
Kufanikisha shughuli za kilimo ni jambo moja na uwepo wa soko la bidhaa zitokanazo na kilimo ni jambo lingine, Na mara nyingi kukosekana kwa masoko ni jambo linalowasumbua sana wakulima na kuwakatisha tamaa ya kuendelea na uzalishaji wa mazao mbalimbali
Kupitia juhudi za Serikali ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya wakulima wa Chunya wametakiwa kuendelea kuiamini Serikali ya awamu ya sita kwani inaendelea kutekeleza yaliyokusidwa kwaajili yao
Katika kuhakikisha soko la ufuta linakuwa sio tatizo, Chama Kikuu cha Ushirika (CHUTCU) kiko tayari kusimamia soko la ufuta Chunya ili kuendelea kuwanufaisha wakulima kama ilivyo kwenye zao la Tumbaku na mazao mengine

Mkuu wa divisheni ya Viwanda, Biashara na uwekezaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Ndugu Lodrick Mwakisole akifafanua jambo ofisini kwake
Mkuu wa divisheni ya Viwanda, Biashara na uwekezaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Ndugu Lodrick Mwakisole amesema kupitia zao la ufuta fursa nyingi za kibiashara zinaendelea kuongezeka Chunya
Mwakisole anawaita vijana wa Chunya na hata watanzania kwa ujumla kuja Chunya kuwekeza kwenye Mnyororo wa kilimo cha ufuta huku akiendelea kuwahimiza wasomi pia kutumia taalum zao kumulika fursa mbalimbali zilizopo ndani ya Chunya
Aidha Mwakisole amesema yeyote anayehitaji kuwekeza kwenye mnyororo wa zao la ufuta na mazao mengine yoyote Chunya Idara yake iko tayari kutoa leseni muda wowote. Pia Divisheni ya viwanda Biashara na uwekezaji ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya iko tayari kutoa usaidizi wowote unaohitaji katika kusajili au kurasimisha biashara za wananchi
Fursa ya kilimo cha zao la Ufuta imefunguliwa Chunya baada ya uwekezaji Mkubwa na juhudi za Serikali ya wilaya ya Chunya kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi kwa wakulima na wanunuzi jambo lililopelekea soko la ufuta kusogezwa ndani ya ardhi ya Chunya tofauti na ilivyokuwa hapo awali
Uliyekosa fursa kwenye zao la Tumbaku na hata mazao mengine sasa umefikiwa kupitia kilimo cha Ufuta, hivyo kazi ni kwako
Kwa undani ya Makala hii unaweza kutazama mtandao wa Youtube kwa kubonyeza kiunganishi hapo chini au Tafuta YOUTUBE Chunya DC online
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.