Waziri Mkuu wa Jamhurinya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Kassim Majaliwa ameagiza kukamatwa na kuwekwa ndani viongozi wa kamati ya watumiaji maji wa mradi wa maji wa Matunguru uliopo katika Kijiji cha Tungamalenga wilayani Iringa kwa tuhuma za ubadhilifu wa sh. milioni saba.
Agizo hilo amelitoa jana Septemba 28, 2019 baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Idodi wilayani Iringa.
Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela afuatilie suala hilo kwa kuwa kamati nyingi za watumiaji maji zimekuwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa kutoka kwa wananchi jambo ambalo sio sahihi.
Alisema ifikapo saa 4.00 asubuhi ya leo watuhumiwa wote wanaohusika na ubadhilifu huo wawe wameshakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola kwa ajili ya kwenda kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Iringa hadi Ruaha yenye urefu wa kilomita 104 ili kuboresha huduma za usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo na kuinua uchumi.
Aliyasema hayo baada ya kupokea malalamiko ya ubovu wa barabara hiyo kutoka kwa mbunge wa jimbo la Ismani, William Lukuvi ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mbunge huyo alisema licha ya Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo ikiwemo ya maji, afya na umeme, lakini wanakabiliwa na tatizo la ubovu wa barabara ambapo aliomba Serikali iwasaidie.
Baada ya Waziri Mkuu kusema kuwa Serikali itahakikisha barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami wananchi walifurahi na kuishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. Rais John Joseph Pombe Magufuli kwa kuwajali wananchi wake.
Awali, Waziri Mkuu alikagua na kuzindua majengo matano ya kituo cha afya Idodi ambayo yamegharimu sh. milioni 400. Pia Serikali iliongeza sh. milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na kusema kuwa ameridhishwa na mradi huo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:OFISI YA WAZIRI MKUU
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.